1. Kuelewa Kwa Kina Kazi za Fasihi
Matumizi ya nadharia katika kuchambua hadithi fupi na riwaya husaidia wachambuzi kuelewa kwa kina kazi hizo. Hii hurahisisha hadhira kuzielewa hadithi fupi na riwaya zisizoeleweka kwa urahisi. Mfano, riwaya za kifalsafa kama Nagona ya Kezilahabi au Babu Alipofufuka ya Said Ahmed Mohamed huwa vigumu kueleweka bila kutumia misingi ya nadharia.
2. Kuboresha Kifani na Kimaudhui
Nadharia zimechangia kuboresha kazi za hadithi fupi na riwaya. Waandishi hutumia misingi ya nadharia mbalimbali kuendeleza vipengele vya fani na maudhui katika kazi zao.
3. Kubaini Utamaduni wa Jamii
Kwa kuwa baadhi ya nadharia za uhakiki kama nadharia ya Uhalisia huweka mkazo katika masuala ya kijamii, uhakiki wa hadithi fupi na riwaya husaidia kubaini utamaduni wa jamii inayosawiriwa. Mfano, riwaya ya Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka ya Aniceti Kitereza inabaini mila na desturi za Wakerewe.
4. Kuchochea Mijadala ya Kijamii
Matumizi ya nadharia za uhakiki yamezifanya hadithi fupi na riwaya kuchochea mijadala ya kijamii kwa kuibua masuala muhimu kama ufisadi, rushwa, wizi, na usaliti. Mijadala hiyo husaidia jamii kufanya mabadiliko chanya.
5. Kuchambua Kitaalamu
Nadharia zimewawazesha wasomaji, wahakiki, na watafiti kuchambua riwaya na hadithi fupi kitaalamu kupitia misingi ya nadharia mbalimbali.
6. Kutoa Mitazamo Mbadala
Nadharia zimesaidia kutoa mitazamo mbadala ya kuelewa hadithi fupi na riwaya. Kila nadharia ina misingi tofauti ambayo hupanua upeo wa kuelewa kazi hizo na kutoa tafsiri tofauti.
7. Kuelewa Kulingana na Wakati na Mazingira
Nadharia zimesaidia kuelewa hadithi fupi na riwaya kulingana na wakati, mazingira, na tamaduni zilizosawiriwa. Hii imezifanya kazi hizo kuwa nyenzo muhimya ya kuhifadhi historia na utamaduni.